Mbinu za kilimo bora cha mboga

MATAYARISHO NA UENDESHAJI WA KITALU CHA MBOGA

Kitalu ni nini?

Kitalu ni mahali ambapo miche huoteshwa na kutunzwa kabla ya kupandikizwa Kwenye bustani au shambani Kwenye mashimo. Mavuno mazuri ya kilimo cha mboga na matunda utategemea sana matunzo bora ya miche kuanzia hatua ya kitalu kwa sababu kitalu ni sehemu mama katika uzalishaji wa miche. Mkulima anapaswa awe mwangalifu katika kuchagua mahali pazuri pa kuweka kitalu. Pamoja na kuwa mwangalifu katika kuchagua eneo linalofaa vile vile mkulima afahamu mbinu za kutayarisha na kutunza miche Kwenye kitalu.

Kuchagua eneo la kitalu

Mambo Muhimu ya Kuzingatia

 1. Eneo la kitalu lisiwe na magugu sugu kama vile ndago na kwekwe.
 2. Usianzishe kitalu kwenye sehemu yenye wadudu au magonjwa ama wanyama waharibifu kama vile panya, nyani, tumbili n.k.
 3. Eneo la kitalu liwe na udongo wenye rutuba, unaohifadhi maji lakini usio tuwamisha maji na udongo usiwe na chumvi chumvi
 4. Eneo la kitalu linatakiwa liwe tambarare, kama ni eneo la milimani, basi ni muhimu kutengeneza matuta ya kitalu kwa kufuata matuta ya mkingamo.
 5. Kitalu kinatakiwa kisiwe mbali sana na bustani halisi ya mboga ili kurahisisha ubebaji na shughuli za kupandikiza miche.
 6. Hakikisha kitalu kipo karibu na njia ili kurahisisha kuleta mbolea, samadi au mboji na pembejeo zingine.
 7. Eneo la kitalu liwe na urahisi wa kupata maji ya kutosha kwa ajili umwagiliaji wa miche. Pawe na kisima au bwawa kwa ajili ya kuhifadhi maji.
 8. Eneo liwe na miti kando kando ya kukinga upepo ili kuzuia upepo mkali Kwenye kitalu.
 9. Eneo la kitalu liwe na mwanga wa jua wa kutosha.

Utayarishaji wa kitalu cha mboga

Mambo muhimu ya kuzingatia

 • Fanya usafi wa kina kwenye eneo ulilolichagua kwa kuondoa vichaka na magugu yote.
 • Hakikisha upatikanaji wa maji kwa kuweka mifereji au njia za kuleta maji au kuhifadhi maji kwa kutengeneza kisima au mifereji.
 • Ni vizuri kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi na kuchanganya mbolea.
 • Hakikisha umelima na kutifua kwa jembe eneo lililotengwa kuoteshea miche.
 • Usisahau Kuangamiza wadudu na magonjwa yatokanayo na udongo kabla ya kutayarisha matuta ya kitalu kwa kutumia madawa ya kunyunyiza katika udongo, kuchoma udongo au kufunika eneo la tuta la kitalu kwa kutumia plastiki inayopitisha mwanga kwa wiki mbili hadi nne ili kuua wadudu na minyoo udongoni.

Aina za matuta ya kitalu

Kuna aina tatu za matuta ya kitalu unayoweza kutengeneza kulingana na msimu na aina ya udongo wa mahali ulipo, tuta la kitalu lililo inuka (tuta n° 1) au tuta la kitalu lililo didimia au jaluba ( tuta n° 2) ama tuta lililo inuka lakini lililobonyea kidogo katikati (tuta n° 3).

1. Tuta lililoinuka na kubonyea katikati

Hili hutumika wakati wa kiangazi sehemu zenye udongo mzito aina ya mfinyanzi unaotuamisha maji ili husaidia kuhifadhi maji.
2. Tuta lililoinuka

Hili hutumika sehemu zenye unyevu na mvua nyingi au sehemu zenye udongo mzito aina ya mfinyanzi unaotuamisha maji ili kuruhusu maji kutawanyika na kwenda chini ya aridhi.
3. Jaruba

Jaruba hutumika sehemu kame au wakati wa kiangazi ili kuhifadhi unyevu wa kutosha katika udongo kwa ajili ya miche.
Upandaji mbegu

Kuna namna mbili za kupanda mbegu kwenye kitalu kama ifuatavyo.

1. Kupanda kwa kutawanya katika tuta.
Kupanda mbegu kwa kutawanya, hufanyika kwa mbegu ndogo ndogo sana kama za mchicha. Ambapo kwa kawaida inashauriwa kuchanganya mbegu hizi na mchanga (katika uwiano wa 1:4) kabla ya kupanda ili kusaidia kuwa na mtawanyiko mzuri wa mbegu katika tuta zima. Baada ya kupanda pitisha reki kuzifukia au mwaga mchanga kiasi juu ya tuta ili kuzifunika.
2. Kupanda kwa mstari
Upandaji wa mbegu kwa mstari unatakiwa kutengeneza mifereji inayo katisha upana wa tuta kwa kutumia kijiti. Mfereji huu uwe na kina kisichozidi sm 2 hadi sm 3. Kupanda mbegu ndogo ndogo kama vile vitunguu, nyanya na kabichi tumia mifereji yenye kina cha sm 2 ili huepusha kuoza kwa mbegu kama zikipandwa chini sana. Weka umbali wa sm 15 hadi 20 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda mbegu katika mstari rudishia udongo na baadaye shindilia udongo ili uweze kushikana na mbegu vizuri.
Mbegu zikishafunikwa kwa udongo, tandaza nyasi juu ya tuta la kitalu ili kuzuia maji kupotea hewani na kukauka kwa tuta na mbegu kabla na baada ya kuota. Kisha mwagilia maji kiasi na baada ya hapo tuta limwagiliwe maji asubuhi na jioni kulingana na hali ya hewa na aina ya udongo. Unaweza kumwagilia maji hadi mara tatu kwa siku kwa sehemu zilizo na jua kali au udongo wa kichanga.

Matunzo ya kitalu

Ondoa nyasi juu ya kitalu mbegu zikishaota. Jengea kichanja kilichotandazwa nyasi au makuti ama kitu chochote ili punguza kupenya kwa mionzi ya jua kwa sababu miche hii bado ni michanga sana hivyo huathirika kwa jua kali ambalo linaweza kuiunguza au kuifanya isikue vizuri. Kichanja kiki kiwe na urefu wa mita moja ili kuwezesha ung’oaji wa magugu na kupunguzia miche bila tatizo lolote. Kichanja hupunguza kasi ya matone ya mvua kubwa ambayo inaweza kujeruhi miche michanga. Kichanja cha kitalu kinaweza kukaa kwa muda wa wiki mbili. Punguza kiasi cha kivuli cha matandazo ya nyasi pole pole na unaweza kutoa kabisa baada ya wiki mbili au tatu.
Miche yenye majani mapana kama vile, kabichi na nyanya, inahitaji kupunguziwa ili kutoa nafasi ya kukua vizuri. Miche ihamishwe mapema maana kuhamisha miche mikubwa ni vigumu zaidi kwa sababu mizizi yake ni mirefu na inaweza kukatika kirahisi.

Utayarishaji wa miche ya kupanda shambani
Ondoa kivuli baada ya wiki mbili au tatu tangu kuota kwa miche ili husaidia miche ianze kuzoea hali halisi ya bustanini hasa jua na upepo mkali. Wiki moja kabla ya kupeleka miche bustanini yaani baada ya wiki
nne kwa mazao mengi ya mboga (kasoro kitunguu wiki 5) punguza kiwango cha maji ya kumwagilia ili miche izoee hali ngumu ya ukame baada ya kupandikizwa bustanini. Miche ipandikizwe ikiwa na udongo kidogo kuzunnguka mizizi yake ili iweze kushika vizuri mara baada ya kupandikizwa shambani.

UTHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU KATIKA MBOGA

Wadudu na magonjwa hupunguza kiasi cha mavuno na hata kuua mimea kabisa, Hupunguza ubora wa mboga, Huongeza gharama za uzalishaji, hasa madawa ya viwandani yanapotumiwa na Huongeza uharibifu wa mboga baada ya kuvuna.
Ni lazima utambue aina ya ugonjwa au mdudu ili utumie kinga Ianayostahili kukabili. Ili kufanikisha lengo hili unaweza kutumia uzoefu wako, hasa baada ya kuwa na wataalam wa wadudu na magonjwa ya mimiea kwa muda mrefu, Kutumia mabwana shamba, Kutumia wataalam wa magonjwa na wadudu wa mboga au kuchunguza sehemu ya mmea uliyougua kwenye maabara.

Kanuni za kukinga mboga dhidi ya magonjwa na wadudu

 • Panda mazao muda unaotakiwa hii itakuwezesha kukwepa baadhi ya magonjwa ya msimu.
 • Usipande mboga ya jamii moja katika eneo moja kwa misimu mingi mfululizo. Changanya mazao au mimea ambayo inafukuza magonjwa na wadudu kama vile mimea inukayo
 • Chagua udongo usiokuwa na magonjwa ya mboga unayotaka kuzalisha.
 • Tumia mbegu bora, kwani baadhi ya magonjwa hutokana na mbegu.
 • Hakiksha kuwa vitalu, bustani na sehemu ya kuhifadhi mboga ni safi kwani uchafu na magugu huvutia magonjwa na wadudu waharibifu.
 • Hakikisha unatoa majani au mimea iliyokwisha ugua, na ichome moto au ifukie..
 • Usichanganye mboga na baadhi ya mazao yanayovutia magonjwa au wadudu katika bustani yako. Mfano mazao kama mipapai na bamia huvutia nzi wadogo weupe wanaoeneza ugonjwa wa “ukoma wa nyanya”.
 • Tumia madawa ya asili na viwandani ili kupunguza kuenea kwa magonjwa na wadudu. Unalazimika kukinga mboga dhidi ya magonjwa na wadudu kwa kutumia madawa ya asili na viwandani pale mbinu nyingine zinaposhindwa kuleta mafanikio.

Kanuni za kukinga magonjwa na wadudu kwa kutumia madawa

Yafuatayonni mambo ya kuzingatia wakati wa kutumia madawa ya asili na viwandani:

 1. Usipige dawa wakati wa upepo mkali au jua kali sana kwani kiasi kikubwa cha dawa kinaweza kupotea hewani.
 2. Usipige dawa wakati wa mvua (mara tu kabla ya mvua) kwani maji ya mvua yataosha na kupunguza nguvu ya dawa.
 3. Unashauriwa kupiga dawa wakati wa asubuhi hasa kukinga magonjwa ya ukungu yapendayo unyevunyevu. Kwa kuzuia wadudu, ni vizuri kupiga dawa wakati wa jioni. Wakati wa jioni dawa huua wadudu zaidi kwani hukaa muda mrefu juu ya majani kabla ya nguvu yake kuharibiwa na jua.
 4. Weka kiwango cha dawa kama ilivyo elekezwa na watengenezaji au watalaam. Kiasi kidogo cha dawa katika maji hufanya viini vya magonjwa na wadudu kuwa sugu.
 5. Kumbuka kuwa kiasi cha sumu ndani ya kasha au kopo la dawa hutofautiana kati ya kampuni na kampuni iliyotengeneza.
 6. Ikiwezekana tafuta ushauri kwa muuza madawa au wataalam waliokaribu nawe.
 7. Hakikisha unapiga dawa ya kutosha sehemu zote za mmea kwani baadhi ya wadudu au magonjwa hukaa na kushambulia sehemu ya chini ya majani.
 8. Andaa vizuri bomba la kupigia dawa kabla ya kuchanaganya dawa na maji ili dawa iweze kutoka vizuri.
 9. Madawa hutofautiana sana nguvu za kuua wadudu, hivyo changua madawa yanayofaa kufuatana na ugonjwa na wadudu.
 10. Unashauriwa kupiga madawa hasa ya viwandani siku 14 kabla ya kuvuna mboga Pamoja na kuepuka kupiga madawa mara kwa mara kwa usalama wa mlaji.
 11. Epuka Kupiga dawa ya aina moja mara kwa mara dhidi ya ugonjwa au mdudu wa aina moja kwa sababu hii kufanya hivyo huwafanya wadudu kujenga sugu dhidi ya dawa hiyo.

Madawa ya asili

Madawa ya asili ni mengi ila bado hajafanyiwa utafiti wa kutosha kuhusu aina ya wadudu na magonjwa ninayotibu, jinsi ya kutumia na kiasi cha kutumia. Baadhi ya mimiea inayotoa madawa ya asili ni mbegu na majani ya muarobaini, tumbaku, pilipili kali, pareto, kitunguu swaumu, manung’anung’a, n.k. Muarobaini ni miongoni mwa mimea michahce ambayo mpaka sasa imefanyiwa utafiti wa kiina. Mfano, kuchanganya nusu kilo ya mbegu za muarobaini zilizotwangwa katika lita ishirini za maji husaidia kuua wadudu mbalimbali wakiwemo funza wanaotoboa matunda ya nyanya.

Madawa ya asili ni bora zaidi kuliko madawa ya viwandani kwani sumu yake ni kidogo na hupungua haraka baada ya kupiga dawa. Hivyo ni salama zaidi kwa mpigaji dawa na mlaji mboga. Hivyo kupendekezwa katika kilimo hai na hifadhi ya mazingira.

Kasoro kubwa katika kutumia madawa ya asili ni kwamba hayajafanyiwa utafiti wa kutosha ukilinganisha na yale ya viwandani. Mfano, nitumie dawa ipi inayofaa kwa mdudu yupi?. Nguvu yake ni kidogo, hayatafaa kuzuia mashambulizi makubwa ya magonjwa au wadudu vilevile yanakinga zaidi mboga dhidi ya wadudu waharibifu kuliko magonjwa.Pia uwiano wa kuchanganya dawa na maji bado haujulikani vizuri. Mfano, niweke kiasi gani cha dawa katika kiasi gani cha maji ?..

Madawa ya viwandani

Madawa ya viwandani yana sumu nyingi zaidi na hivyo huzuia haraka zaidi mashambulio ya magonjwa na wadudu. Hivyo, hutumika sana katika kilimo cha mboga na mazao mbali mbali kuliko madawa ya kienyeji. Changamoto la haya madawa ni kwamba ni hatari kwa mkulima, mlaji wa mboga, mazingira na pia gharama zake ni kubwa.

KUVUNA NA KUHIFADHI MBOGA

Uvunaji wa mboga

Uvunaji wa mazao ya mboga ni hatua ya mwisho na muhimu sana katika uzalishaji. Kabla ya kuchukua uamuzi wa kuvuna mboga ni muhimu kufanya utafiti wa soko la mavuno hayo, kutafakari na kuchagua aina au njia ya kuvuna na kusafirisha mazao hadi kwenye soko. Ni muhimu kupanga mipango hii mapema ili pindi zao linapokomaa uvunaji ufanyike na hivyo kuepuka zao kubakia bustanini kwa muda mrefu ambao utasababisha kuharibika.

Unapaswa kuwa makini sana katika mipangilio ya shughuli zake ili kujipatia mavuno mengi na bora na baadaye kuweza kuyauza kwa bei nzuri.

Jinsi ya kutambua ukomavu unaofaa kwa kuvuna mboga za aina mbali mbali.
Dalili au kipindi cha ukomavu unaofaa kwa kuvuna mboga maranyingi hutokana na uzoefu wa mkulima mwenyewe pamoja na mahitaji ya soko, umbali wa kusafirisha mboga na aina ya usafiri utakao tumika kusafirisha mboga. Kumbuka kuwa mboga ni mazao yasiyoweza kuhifadhika kwa muda mrefu na yanahitaji kutumiwa haraka mara tu baada ya kuvunwa.

Uvunaji wa mboga mboga

Dalili za mboga iliyo tayari kuvunwa inategemea aina ya zao lenyewe. Kwa mfano mboga za majani kama vile mchicha, chainizi kabichi, inatakiwa iwe na majani teke yasiyo komaa sana. Mchicha usiwe umeanza kutoa hata lile ua la kwanza. Chainizi ivunwe kabla ya majani yake kuwa na miiba/manyoya na pia majani hayatakiwi kutoa nyuzi yanapochunwa.

Uvunaji wa kabichi

Kabichi inafaa ivunwe wakati ikiwa imefunga vizuri na kuwa ngumu inapo kubonyezwa kwa kidole gumba. Pia iwapo utaipiga kwa mkono inatoa mlio wa ngoma. Kabla ya kuonyesha dalili hizi basi kabichi itakuwa bado haijakomaa. Na madhara yake ni kunyauka mapema baada ya kuvunwa.

Uvunaji wa mboga za matunda

Uvunaji wa Mboga za matunda kama vile ngogwe, biringanya na bamia zivunwe wakati ngozi yake ikiwa ni ng’aavu na laini. Hapo mbegu zilizomo ndani bado hazijakomaa na hivyo ni laini kwa kula. Baadaa ya hapo hugeuka rangi na kuwa njano (mfano ngogwe na biriganya) au kupoteza ung’aavu wake. Hapo mbegu huwa zimekomaa na hazifai tena kwa soko. Wakati mwingine uvunaji wa biringanya au ngogwe unaweza kufanyika zingali changa, hii yaweza kufanyika kama kuna mahitaji maalum ya mteja wa mboga ya aina hii. Hapo unaweza kumvunia mteja kwa makubaliano.

Uvunaji wa nyanya uko katika aina mbili: (1) Unaweza kuvuna nyanya mbichi kidogo kwa ajili ya mahitaji maalum ya mteja au kama unasafirisha mbali na hivyo ziweze kufika zikiwa na hali nzuri na kuiva taratibu safarini pasipo kuharibika. (2) Unaweza kuvuna nyanya zilizo iva kabisa, hizi zivunwe kama soko ni la karibu au kwa mauzo ya hapo hapo ili kuepuka uharibifu safarini na mara zikiwa sokoni.

Mazao ya mbogamboga za mizizi

Mazao ya mboga za mizizi kama vile karoti yavunwe yakiwa teke lakini yamekomaa, kabla ya kuwa na nyuzi nyuzi au kamba kamba. Karoti iwe imefikia ukubwa unao takiwa na kabla haija jaza maji na kupoteza utamu au sukari. Sehemu ya katikati ya karoti isiwe kubwa na isiwe imejaa maji.

Mboga zinazovunwa zinatakiwa ziwekwe mahali penye kivuli cha kutosha na unyevu pasipo na jua kali ili zisinyauke. Inapendekezwa, mboga zivunwe kipindi cha asubuhi na siyo wakati wa jua kali. Isipokua mboga jamii ya vitunguu ambavyo huhitaji kukaushwa ili kuhifadhika vizuri.

Uhifadhi wa mboga

Jinsi ya kuhifadbi mboga baada ya kuvuna
Unaweza kupunguza kuharibika kwa mazao ya mboga kwa njia zifuatazo

 • Unatakiwa kuvuna mboga mbichi asubuhi na mapema kabla jua halijawa kali ili kupunguza uharibifu utokanao na joto kali linalo sababishwa na jua.
 • Hakikisha unaosha mboga zako mara baada ya kuvuna ili kupunguza joto la jua, hasa endapo umevuna wakati wa jua kali.
 • Hakikisha unahifadhi mboga mahali pasafi ili kuepuka maambukizo ya magonjwa ya kuozesha mboga.
 • Hifadhi mboga zilizovunwa katika sehemu ya baridi au kivuli na yenye unyevu wa kutosha. Hata hivyo vitunguu huhitaji kuhifadhiwa sehemu kavu ili visiote.
 • Wakati wa kusafirisha, panga mboga katika vyombo imara vyenye ujazo mdogo mfano wa makasha, badala ya kushindilia katika matenga, magunia, viroba au kumwaga katika gari/lori.
 • Epuka kupakia mboga kupita kiasi katika matenga au magari ya kusafirishia ili hupunguza mgongano au mbanano wa mboga ambao unaweza kusababisha vidonda na kuoza kwa mboga haraka.
 • Nyunyizia maji kwenye mboga hasa mboga za majani ili zisinyauke na kuharibika haraka.

Sababu za mboga kuharibika

 1. Umbali kati ya masoko na sehemu ya uzalishaji.
 2. Ubovu wa miundombinu ya usafirishaji kama barabara na upungufu wa vyombo vya usafiri.
 3. Msuguano au mbanano ambao husababisha mikwaruzo na vidonda kwenye mboga. Hii husababishwa na kupakia mboga kupita kiasi na bila mpangilio katika matenga au magunia.
 4. Joto kali na hewa kavu ya kuhifadhi husababisha mboga mbichi kupoteza maji mengi sana na hata kunyauka kabla ya kuuzwa.
 5. Mashambulizi ya magonjwa na wadudu mbalimbali baada ya kuvuna husababisha mboga kuharibika au kuoza.
 6. Namna mbaya ya Upangaji na upakiaji wa mboga katika vyombo vya kusafirishia.

Upangaji wa mboga katika vyombo vya kusafirishia

Unashauriwa kupanga mboga vizuri katika vyombo vya kusafirishia ili kupunguza uharibifu wa mboga kwa njia ya mgandamizo na msuguano na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa na hivyo kupunguza uwezekano wa kuoza kwa mboga. Vile vile kupanga vizuri mboga hufanya bidhaa kuvutia zaidi wateja.

Aina za vyombo/vifaa vya kusafirishia mboga

Unashauriwa kuchagua vifaa vya kuhifadhia mboga kufuatana na upatikanaji na gharama za vyombo hivyo, aina ya mboga na usafiri.
1. Makasha ya mbao au plastiki huweza pia kutumika badala ya matenga kuhifadhia mboga zinazoharibika haraka zaidi kama vile nyanya, pilipili hoho, n.k. Makasha ni mazuri kwani hupunguza uharibifu wa mboga unaotokana na mbanano kati ya kasha na kasha. Pia kwa kuwa makasha yanamatundu, husaidia kupunguza joto kali ndani ya kasha na mboga.
2. Magunia, viroba na mapakacha hufaa zaidi kwa mboga zote ambazo haziharibiki haraka kama vile vitunguu, vitunguu swaumu, kabichi, ngogwe, karoti, viazi vitamu na mviringo, n.k.
3. Matenga hufaa kutumika kusafirishia mboga ambazo huharibika haraka kama vile nyanya, bilinganya, ngogwe, chainizi, swisichardi, pilipili hoho, n.k. Licha ya kuwa na matundu ya hewa (kupunguza joto), hata hivyo matenga siyo mazuri kusafirishia mboga laini kwani husababisha uharibifu mkubwa wa mboga kutokana na mgandamizo kati ya tabaka na tabaka na pia kati ya tenga na tenga.

Madaraja ya ubora wa mboga

Haya huitwa pia ‘gredi’. Kupanga mboga katika gredi ni muhimu sana hasa katika masoko ya ushindani. Husaidia kufanya bidhaa ivutie zaidi wateja na hivyo basi kuuzika kirahisi.

Vigezo vya kutumia wakati wa kugredi mboga
Vigezo hivi viko vingi na vinategemea hali ya soko la mboga. Vigezo vikuu ni kama ifuatavyo.

 • Ukubwa wa matunda, majani, viazi, vitunguu au karoti.
 • Rangi ya matunda na majani.
 • Usafi wa mboga. Mboga zilizooshwa huvutia zaidi wateja.
 • Maumbile ya matunda au tunguu.
 • Kiwango cha ukomavu wa matunda.

KILIMO CHA MATONE (DRIP IRRIGATION)

Hii ni njia ya kumwagilia mmea kwa kutumia tone(matone) la maji kwa muda husika, ambapo bomba dogo huundwa kwa kuwekewa matundu madogo madogo kwa kuzin¬gatia mmea ulipo kwaajili ya kuupa maji mmea muda wote, Umwagiliaji huu unaweza kuendeshwa kwa mashine au kwa mkono. Umwagiliaji huu pia unaweza fanyika kwa mazao yaliyo mengi ikiwemo ya mboga mboga, matunda na hata nafaka. Katika maeneo yaliyo mengi umwagiliaji huu wakulima hupendelea kuufanya kwa mazao ya matunda na mboga mboga.

Faida za umwagiliaji wa matone

 1. Mgawanyo wa maji katika mimea ni sawa.
 2. Mmonyoko wa udongo ni mdogo sana.
 3. Hupunguza gharama za wasaidizi shambani.
 4. Huokoa muda.
 5. Matumizi ya maji ni yenye mafanikio.
 6. Mavuno ni ya uhakika

Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza umwagiliaji wa ma¬tone

Aina ya udongo.
Aina ya udongo ni muhimu sana kujua aina kama ni tifutifu, kichanga au mfinyanzi,hii itakusaidia mkulima kujua uwezo wa aina husika ya udongo wa kuhifadhi maji ardhini.
Nafasi katika upandaji.
Kila zao lina nafasi zake katika upandaji hivyo unavyoweka mfumo wa umwagiliaji hakikisha nafasi unazo weka ziendane na nafasi ya zao husika.

Topografia
Huu ni umwagiliaji wenye mafanikio hakikikisha eneo lako lipo tambarare, hata kama mteremko utawepo uwe mteremko wa wastani, kufanya mgawanyo wa maji kuwa sawa. Pia zingatia sehemu ya kuweka chanzo cha maji inaweza kuwa ni pipa liliweke¬wa miundo mbinu mizuri miundombinu hiyo kama bomba zilizo sanifiwa vyema kufikia kwenye mmea, pipa au chanzo chochote cha maji hicho kiwekwe sehemu iliyo inuka ili kufanya maji yateremke vizuri kwenye bomba mpaka kwenye mmea.
Mgawanyo wa maji.
Maji ni lazima yawe yenye ubora na maji yawe ya uhakika, kwa kuzingatia hilo pia topografia ya eneo husika ni iwe tambarare au mteremko kiasi Kuruhusu maji ku gawanyika vyema kwenye mmea kwa kiwango kile kile na spidi ile ile kwa kila mmea.

Changamoto za umwagiliaji wa matone

Kama maji yatakayo tumika katika umwagiliaji yakiwa na chumvi husababisha udongo kuwa na chumvi. Kama miundombinu haitawekwa sawa upotevu wa maji utakuwa mkubwa.

Jinsi ya kuweka mfumo wa umwagiliaji shambani

Vitu vifuatavyo viwepo; vifaa, chanzo cha maji,ukubwa wa shamba.
Katika umwagiliaji huu vifaa vinavyoweza tumika ikiwemo,
Chanzo cha maji
kinaweza kuwa pipa, hakikisha pipa hili limetobolewa na kupitisha maji mpaka kwenye bomba ambazo zitakuwa zimewekwa moja kwa moja kwenye mmea. ii.
Bomba
Hizi ziwe zimetobolewa kulingana na nafasi kutoka mmea hadi mmea, na zimewekwa kulingana na mstari kama mistari ipo kumi na bomba ziwe kumi. Sehemu za mfumo huu wa umwagiliaji
Vali(valvu)
Kazi ya hichi chombo ni kuruhusu maji yatoke au yasitoke, ni sawa sawa na koki kama wengine wanavyoita.
Kichujio
Ni muhimu sana kwani itasaidia kuchuja maji kuzuia uchafu kama mchanga, nyasi ambazo huenda zikasabibisha matundu yakutolea maji kuziba, hizi chujio ziwek¬we kabla ya kufungwa bomba za kupeleka maji kwenye mmea.
Emmita:
Haya ndio matundu ambayo yanapeleka maji kwenye mmea, kwa kawaida hutoa maji kwa muda wa saa moja kwa maji lita 4 kwa gallon moja la maji.

Uendeshaji wa mfumo huu wa umwagiliaji Mfumo huu uendeshwe kwa kuzingatia maji yanafika katika mmea husika kwa kiwango kile kile kwa mimea yote Hakikisha hakuna upotevu wa maji kama bomba zinavuja hakikisha hazivuji. Mfumo huu kuwa wenye mafanikio yapaswa ukaguzi wa mara kwa mara ili kuangalia unavyo fanya kazi.

Aidha hakikisha maji yanafika katika mmea kama inavyotakiwa. Na kabla hauja upeleka katika utekelezaji mfumo huu shambani chora kwanza ramani katika katika karatasi halafu nenda ukauweke shambani.

Shopping Cart
0
  0
  Your Cart
  Your cart is emptyReturn to Shop
  × Click here to chat with us